Serikali imeruhusiwa kurekebisha mpaka wa Pori la Akiba la Selous ambalo ni eneo la urithi wa dunia kwa ajili ya kuruhusu uchimbaji wa madini aina ya urani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameyasema hayo Dar es Salam wakati anazungumzia kikao cha 36 kinachoendelea katika Jiji la Saint Petersburg nchini Urusi kilichokutanisha Kamati ya Urithi wa Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Balozi Kagasheki amesema katika kikao hicho, Tanzania iliwasilisha tena ombi lake la kutaka kurekebisha mpaka wa Pori hilo la Selous ambalo lina ukubwa wa asilimia 0.8 sawa na kilometa 200.
Balozi Kagasheki amesema kutokana na kukubaliwa ombi hilo, itakuwa ni fursa nzuri ya kutimiza malengo ya taifa kiuchumi na kijamii kwa wananchi pamoja na kulihifadhi eneo litakalobaki na kuliendeleza.
Pori hilo la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000, na ni mojawapo ya hifadhi kubwa duniani zenye viumbe mbalimbali.
Ni eneo maarufu kwa nyanda kubwa za tambarare zenye nyasi na misitu ya miombo pamoja na aina nyingi za wanyamapori.
Wakati huo huo, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa juu ya utalii endelevu pamoja na kulinda maeneo ya hifadhi ambalo litafanyika Oktoba 15 hadi 19 mkoani Arusha.
0 comments:
Post a Comment